Msomaji wa Biblia.

Utangulizi

Kitabu hiki kinahusu hotuba iliyotolewa mbele ya wabunge, maprofesa wa vyuo vikuu, waandishi wa habari na wafanyabiashara, kwenye bunge ya Bulgaria. Baadaye maelezo ya hotuba hii yalichapishwa katika gazeti kubwa la kila siku la Bulgaria liitwalo ‘TRUD’, la tarehe 3 Marchi, 2001. Nakala laki tatu arobaini elfu za gazeti hili zilichapishwa siku hiyo. Katika hotuba hii Profesa. Dr. Detschko Svilenov anaonyesha msimamo wa Biblia kuhusu Wakati uliopita, uliopo na ule ujao wa wanadamu. Mtoaji wa hotuba hii pamoja na marafiki wake, wameamua kuichapisha hotuba hii kwa lugha mbalimbali kutokana na kuelewa umuhimu wa kila mtu kujua mambo yaliyozungumziwa katika mada hii likiwemo lile la mwisho ya dunia. Hebu sasa fuatana na profesa Dr. Detschko Svilenov katika hotuba yake aliyoitoa mwezi Julai mwaka 2000.

Ndugu waheshimiwa Mabibi na Mabwana,

Mwaka 2000 mamilioni ya watu walikusanyika duniani kote, kumkumbuka mtu mashuhuri aliyebadilisha maisha ya watu wengi kutokana na kujitoa kwake. Katika kumbukumbu hiyo, watu waliimimina mioyo yao kumshukuru mtu huyo kutokana na kusababisha mabadiliko makubwa katika maisha yao. Niwe wazi zaidi kusema kuwa, ujio wa Yesu Kristo duniani ndilo tukio kubwa kuliko matukio mengine yote yaliyowahi kutokea katika historia ya mwanadamu. Ni uumbaji wa mwanadamu peke yake ndio unaoweza kulinganishwa na tukio hili. Miaka elfu mbili iliyopita, mtu huyu mashuhuri alizaliwa kwa njia isiyo ya kawaida. Kuzaliwa kwake kulitabiriwa na manabii miaka maelfu huko nyuma, na ulimwengu ulikuwa unamngojea kwa hamu kubwa. Baada ya kuzaliwa aliishi maisha ya kawaida, akifanya kazi kwa uaminifu na jamaa zake walikuwa watu wa kawaida.

Ingawa mtu huyu hakuwahi kukuandika kitabu cho chote, vitabu vilivyoandikwa juu yake ni vingi kuliko vile vilivyoandikwa kuwahusu watu wengine mashuhuri katika historia ya mwanadamu. Hotuba zake zimehifadhiwa kwa karne nyingi kama urithi mkamilifu kwa wanadamu. Maneno yake ni uzima, yanafanya kazi na yametafsiriwa na kuenezwa ulimwenguni kote katika lugha na ndimi zaidi ya elfu nne. Kama hili halitoshi, zaidi ya watu bilioni moja wamejiweka chini ya uanafunzi wake licha ya kuwa katika kuishi kwake, hakuwahi kuanzisha chuo cho chote. Yesu Kristo hakuwa mkandarasi wa majengo, lakini majengo mengi makubwa na ya kuvutia yamejengwa kwa ajili yake. Amewavutia wanamuziki mashuhuri duniani kutunga kutengeneza muziki unaohusu tabia, mwenendo na nguvu ya maneno yake, licha ya kuwa yeye mwenyewe hakuwa mwanamuziki.

Mtu huyu alikuwa sio daktari, lakini aliponya na anaendelea kuponya watu walio na magonjwa ya kila aina. Hali kadhalika, ulimwengu umejaa kazi za kuvutia za kisanii zinazohusisha maisha yake na kazi zake, licha ya kuwa hakuwa msanii. Yesu Kristo hakuwa ‘Jenerali’, lakini ana majeshi mamilioni kwa mamilioni katika kila nchi duniani. Sambamba na mabadiliko haya yaliyotokana na ujio wake, historia ya wanadamu nayo imegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni maisha kabla ya Kristo (K.K), na maisha baada ya Kristo (B.K). Shuhuda hizi kuhusu ukuu wake zinaonyesha upekee usio na mipaka wa udhihirisho wa nguvu na mamlaka yake.

Kutokana na mabadiliko yaliyosababishwa na maisha ya mtu huyu, watu wengine katika miaka tuliyo nayo wanamwangalia kama mleta mabadiliko na maendeleo katika jamii. Ukiangalia jinsi wanadamu walivyoishi kabla ya Kristo, utakubaliana na ukweli huu kwa asilimia mia moja. Maisha ya wanadamu na ustaarabu wake yanawiwa naye kutokana na mafundisho yake kuwa sababisho la kukomeshwa kwa biashara ya utumwa, pamoja na kurejesha hadhi na heshima ya wanawake. Kabla ya ujio wake dini na jamii nyingi zilikuwa zinamchukulia mwanamke kama chombo cha kuzaa na kutumiwa tu. Lakini Yeye alipokuja alisema; “…Hakuna mwanamume wala mwanamke, maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu” (Wagalatia 3:28).

Pasipo shaka yoyote, maadili ya Kikristo yamesababisha mtizamo wa jamii kuhusu mwanamke kubadilika na kuwa bora zaidi. Kutokana na mabadiliko ya kidemokrasia yanayoendelea katika mataifa mbalimbali, maendeleo na usitawi katika kila nchi yanapimwa kwa kuangalia nafasi za wanawake kiutawala katika nchi au jamii husika.

Mtu yeyote mwenye mashaka anatakiwa kutambua kuwa sayansi, mahakama, dini, sanaa, historia, falsafa pamoja na mambo mengine yanayohusu ustaarabu wa mwanadamu, vinashuhudia upekee wa uwezo na mvuto wa Yesu Kristo katika jamii. Kama vile Mungu asivyo na mwanzo wala mwisho, ukuu wa Yesu Kristo nao hauna mwisho. Mashirika mbalimbali vya kijamii duniani yanathibitisha kuwa rehema na udugu wa kipekee katika kuhudumiana kwa kiwango kikubwa ni matunda ya Ukristo. Pasipo shaka yoyote waanzilishi wa shirika kubwa duniani linalotoa misaada ya kibinadamu la Msalaba Mwekundu, waliongozwa na Roho Mtakatifu na mafundisho ya Yesu Kristo, kuchagua alama ya Kikristo kuwa ni nembo ya shirika lao. Yesu alitupatia kanuni ya msingi kuhusu maisha ya kuhudumiana pale aliposema, “Yoyote mtakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo” (Mathayo 7:12). Hali kadhalika katika waraka wa Warumi tunakutana na maneno yasemayo, “Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe” (Warumi 12:20).


Yaliyomo

Download

Image:product

Kitabu hiki kinapatikana bila malipo kwenye faili zima: PDF | ZIP